LHRC yaiomba Tume ya Haki za Binadamu Afrika kuishauri Tanzania Kuheshimu na Kufuata Haki za Binadamu

LHRC yaiomba Tume ya Haki za Binadamu Afrika kuishauri Tanzania Kuheshimu na Kufuata Haki za Binadamu

Posted tokea miaka 6

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kimeshiriki na kuwasilisha mapendekezo juu ya hali ya haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania katika Mkutano wa 63 wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Afrika unaofanyika mjini Banjul, Gambia kuanzia tar 24 oktoba 2018.

Akisoma mapendekezo hayo ya asasi za kiraia mbele ya Mwenyekiti wa Tume na washiriki kutoka taasisi mbalimbali  za kimataifa, mwakilishi wa LHRC Bw. William Kahale amesifu utendaji wa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, juu ya vita dhidi ya rushwa na kuongeza uwajibikaji serikalini.

Pamoja na hayo, Kituo kimependekeza na kuiomba Tume ya Haki za Biandamu na Haki za Watu ya Afrika kuishauri serikali ya Tanzania kuondoa vikwazo juu ya uhuru wa kujieleza na kutoa taarifa na uhuru wa kukusanyika ambao  hivi karibuni umekua ukitishiwa kutokana na uwepo kwa sheria kandamizi ikiwemo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Kanuni za Maudhui ya Mitandaoni za mwaka 2018, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

Pia, LHRC imependekeza kuondolewa wa vikwazo dhidi ya shughuli za kisiasa kwa vyama vya siasa hususani vyama vya upinzani, ambapo kwa kiasi kikubwa vimewekewa makatazo ya kufanya mikutano yao kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mikataba ya ya Kimataifa hususani Mkataba wa Umoja wa Afrika.

Pamoja na hayo, Kituo kimeomba kamisheni iishauri serikali ya Tanzania kuondoa amri ya kutoruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kurejea masomoni wanapojifungua, ambayo inalenga kumkandamiza mtoto wa kike katika kufurahia haki yake ya elimu.

Sambamba na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, nchi ya Tanzania imewakilishwa na asasi za kiraia 18, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika, Kituo cha Sheria Zanzibar, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Mtandao wa Watoaji wa Msaada wa Sheria, Baraza la Habari Tanzania na nyinginezo.

Imetolewa Oktoba 25 na;

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu