KUSIKITISHWA NA TUKIO LA MOTO LILILOTOKEA KATIKA SOKO KUU LA KARIAKOO

KUSIKITISHWA NA TUKIO LA MOTO LILILOTOKEA KATIKA SOKO KUU LA KARIAKOO

Posted tokea miaka 3

TAARIFA KWA UMMA

 

KUSIKITISHWA NA TUKIO LA MOTO LILILOTOKEA KATIKA SOKO KUU LA KARIAKOO

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesikitishwa na tukio la moto lililotokea katika Soko Kuu la Kariakoo na kusababisha uharibifu wa vitu mbalimbali vyenye thamani. Pia tunachukua fursa hii kuwapa pole wote walioathirika na tukio hili kwa namna yoyote.

Tunaipongeza Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Mhe. Kassimu Majaliwa, kwa kuunda Kamati ya kuchunguza chanzo cha moto huo na kutoa majibu haraka iwezekanavyo.

Kituo kimesikitishwa na kuchelewa kwa kikosi cha zimamoto kufika eneo la tukio na hivyo moto kuteketeza soko hilo. Matukio ya moto yamekithiri sana katika kipindi cha karibuni ambapo maeneo mbalimbali yakiwemo mashule yameweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kupoteza maisha na uharibifu wa mali katika mikoa mbalimbali.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito kwa Serikali na wadau kuendelea kutoa elimu ya majanga na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayaendelei kutokea nchini na kusababisha hasara kwa wananchi. Hii ni kwa sababu ni matukio ambayo yanazuilika kukiwepo na mikakati thabiti ya kujiandaa na matukio kama haya.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaamini kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu itakuja na majibu na mapendekezo ambayo yatasaidia kuepuka matukio kama haya katika siku za mbele.

 

Imetolewa leo tarehe 12/07/2021 na;

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Anna Henga (Wakili)

Mkurugenzi Mtendaji