
KESI YA KUPINGA SHERIA NA KANUNI ZA TOZO KATIKA MIAMALA YA SIMU
TAARIFA KWA UMMA
KESI YA KUPINGA SHERIA NA KANUNI ZA TOZO KATIKA MIAMALA YA SIMU
Siku ya tarehe 27/07/2021 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilifungua shauri la namba 11 ya mwaka 2021 kuomba Mapitio ya Mahakama Kuu (Judicial Review) kuhusu National Payments System Act Cap. 437 pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu. Kesi imetajwa kwa mara ya kwanza tarehe 05/08/2021 mbele ya Mh. Jaji John Mgeta.
LHRC kimefungua kesi hiyo kufuatia kupitishwa kwa mapendekezo ya Bajeti ya Serikali 2021/22 pamoja na sheria ya fedha ilipelekea kuweka tozo katika miamala ya fedha inayofanywa kwa njia ya simu, jambo ambalo limeongeza mzigo kwa mwananchi wa kawaida pamoja na wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilifanya uchambuzi wa hotuba ya bajeti iliyowasilishwa mnano tarehe 10/06/2021 na Waziri wa Fedha na Mipango Mh. Mwigulu Nchemba kuhusu athari ya tozo katika miamala ya simu kwa wananchi ambapo mapendekezo hayo yalirudiwa tena baada ya kuletwa kwa madiliko ya sheria ya fedha.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itasikiliza tena kesi hiyo kwa mara ya pili siku ya tarehe 16/08/2021.
Imetolewa leo Agosti 06, 2021 na;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
Bi. Anna Henga
Mkurugenzi Mtendaji