LHRC HQ: Justice Lugakingira House
+255 22 2773038 / +255 22 2773048

Nyamuma Iliyobaki

  • Nyamuma Iliyobaki

NYAMUMA ILIYOBAKI


Organization Report

Report attachment

Download

Kuvamiwa na kuondolewa kinguvu kwa wakazi wa iliyokuwa Nyamuma ni ukatili na uvunjifu mkubwa wa Haki za Binadamu uliotokea katika Kijiji cha “Nyamuma Iliyobaki”. Kijiji hiki kilikuwa kinapakana na pori la akiba la Ikorongo, pembezoni mwa hifadhi ya Serengeti.

Ikumbukwe kuwa, wakazi wa kilichokuwa kijiji cha Nyamuma waliishi maeneo hayo kwa miaka mingi tena bila bughudha yoyote hadi ilipofikamwaka 1994, ambapo uongozi wa Wilaya ya Serengeti uliamua kuongeza mipaka ya pori la akiba la Ikorongo. Matokeo yake ni kuwa sehemu kubwa ya Kijiji cha Nyamuma ilitwaliwa na kujumuishwa katika pori la akiba la Ikorongo na kubaki eneo dogo tu la makazi ya watu, waliloliita “Nyamuma Iliyobaki”.

Watu hawa wa “Nyamuma Iliyobaki” waliendelea na maisha kwa amani wakijihusisha na shughuli zao za uzalishaji kama kawaida, hadi mwezi Oktoba, 2001 ambapo lilitolewa tangazo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya (wakati huo akiwa ndugu Thomas Ole Sabaya) kuwataka wakazi wa “Nyamuma Iliyobaki” kuondoka katika makazi hayo haraka iwezekanavyo.

Siku mbili tu baada ya tangazo la Mh. Mkuu wa Wilaya, kilifika kikosi kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya mwenyewe, akiambatana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Serengeti (OCD), ndugu Alexander Pantaleo Lyimo na kusimamia zoezi la kuwaondoa wakazi wa “Nyamuma Iliyobaki”.

 

Zoezi hilo lilikuwa la kimabavu na kikatili, kwani watu walipigwa, nyumba zao zilichomwa moto, mifugo na mazao kuteketezwa kwa moto. Watu walikimbia hovyo kujinusuru, familia zilisambaratika kwa kupotezana na wengine wamepotea hadi leo wasijulikane walipo.

Kwa zaidi ya miaka 19 sasa, waathirika hawa wamekuwa na safari ndefu ya kutafuta haki ya kuwa na kwao na haki nyingine za msingi zimpasazo mwanadamu kuwa nazo, bila mafanikio.

Hata hivyo, kupitia juhudi za watu mbalimbali, hususan Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mwangaza umeanza kujitokeza mwishoni mwa handaki.

Pamoja na jitihada hizi, haki za watu hawa kucheleweshwa kwa muda wote huu, ni haki za watu hawa kunyimwa.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeamua kuweka katika maandishi kisa hiki ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kazi iliyozifanya kwa kipindi kirefu na kwa wakati huu wa kuadhimisha miaka 25 tangu kianzishwe kumbukumbu hii itasaidia kuonyesha umuhimu wakufuatilia haki kwa kila hali na zaidi kuonyesha kuwa haki ikiminywa bila juhudi, kuipata si rahisi. Kwa jamii ya haki na usawa haki ni lazima zifuatiliwe.